January Makamba (MB),
S.L.P 29,
Simu: +255 767 78 39 96
Nukushi: +255 22 2601066
BUMBULI - LUSHOTO
3 Februari, 2011.
Mheshimiwa William M. Ngeleja (MB)
Waziri wa Nishati na Madini
S.L.P 2000,
Dar es Salaam.
Mheshimiwa Waziri,
YAH: TAARIFA YA SERIKALI BUNGENI KUHUSU UMEME NCHINI
Nakuandikia kwa heshima na taadhima, Mheshimiwa Waziri, kutimiza wajibu wangu kama Mtanzania, kama kiongozi na mwakilishi wa watu, na kama mjumbe katika mhimili wenye wajibu wa kikatiba wa kuishauri na kuisimamia Serikali, kutoa ushauri kwamba ingekuwa manufaa kama Serikali, kupitia Wizara yako, ingetoa Taarifa ya Serikali Bungeni yenye ufafanuzi wa kina kuhusu masuala yote makubwa na yenye utata yanayohusu sekta ya nishati nchini ili kuweka rekodi sahihi kuhusu mambo hayo, kuelimisha umma kuhusu jitihada za Serikali kutatua matatizo ya umeme nchini, na kuondoa shauku ya Watanzania kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini sasa na kwa siku zijazo. Kama itakupendeza na kama itaipendeza Serikali, nashauri Taarifa ya Serikali ijumuishe, pamoja na mambo mengine ambayo Serikali itaona ni muhimu, masuala yafuatayo:
1. Maelezo kuhusu kesi mbili zinazohusiana na mkataba wa uzalishaji wa umeme wa IPTL zilizofunguliwa na Benki ya Stardard Chartered (Hong Kong) dhidi ya Serikali na TANESCO kwenye kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Kesi za Uwekezaji (International Centre for the Settlement of Investment Disputes - ICSID), mahakama ambayo ni kitengo cha Benki ya Dunia (World Bank). Kesi hizo, ICSID Case No. ARB/10/20 dhidi ya TANESCO iliyofunguliwa tarehe 1 Oktoba 2010 na ICSID Case No. ARB/10/12 dhidi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofunguliwa tarehe 11 Juni 2010, zinaweza kuwa na madhara makubwa kwa umma na zinaweza hata kuigharimu Serikali pesa nyingi kuliko zinazodaiwa katika kesi ya Dowans. Taarifa ya Serikali Bungeni itatoa fursa kwa Serikali kuujulisha rasmi umma kuhusu kesi hizi, nini kinadaiwa dhidi ya TANESCO na Serikali pamoja na maandalizi ya Serikali kushinda kesi hizi ili kuepukana na marudio ya dhahama ya Dowans. Vilevile, kama utaona inabidi, basi fursa ya Taarifa ya Serikali inaweza pia kutumika kuwajulisha wananchi sababu za Serikali kutotoa taarifa za kesi hizi mbili muhimu kwa maslahi ya umma hadi sasa.
2. Mheshimiwa Waziri, naamini unafahamu kwamba tangu mwaka 2006, zimetoka ahadi na matamko sita ya Serikali ya kumaliza tatizo la mgawo wa umeme nchini, lakini hadi sasa bado mgawo unaendelea. Ingawa kila mara kunapotokea mgawo mpya, kumekuwa na maelezo na sababu za mgawo huo, lakini mara zote maelezo au sababu hizo huwa zinajirudia. Wewe mwenyewe, Mheshimiwa Waziri, pia umetoa ahadi kadhaa za kumaliza tatizo hili, lakini ahadi hizo hazikutimia. Matokeo ya hali hii ni wananchi kupoteza imani na uwezo wa Serikali yao kutatua tatizo la umeme nchini na hata matatizo yao mengine. Kuna gharama kubwa kwa wananchi kupoteza imani na Serikali yao. Mimi naamini kwamba Serikali ikitoa Tamko la dhati kabisa Bungeni linalobainisha kwa kina na kwa uwazi sababu za ahadi hizi za mara kwa mara kutotimizwa na hatua zinazochukuliwa kuzuia ahadi zinazotolewa sasa na zitakazofuatia kutokumbwa na vikwazo vilivyosababisha ahadi za nyuma zisitimizwe, basi tutakuwa tumepiga hatua kwenye kuimarisha imani ya wananchi kwa Serikali yao.
3. Mtambo wa IPTL unaozalisha umeme kwa kutumia mafuta mazito aina ya HFO unaigharimu Serikali mabilioni ya shilingi kwa mwezi licha ya kuzalisha umeme chini ya nusu ya uwezo wake, hasa kutokana na uhaba na bei kubwa ya mafuta – gharama kubwa kiasi kwamba Serikali imeamua kulipia gharama zote za kubadilisha au kukarabati mitambo hiyo, ambayo sio mali yake bali ya IPTL, ili itumie gesi asilia badala ya mafuta mazito ya HFO. Mwaka 2006, Serikali iliingia mkataba na kampuni ya Alstom Power Rentals kuzalisha umeme Mkoani Mwanza kwa kutumia mitambo ya mafuta. Kutokana na shida na gharama kubwa ya upatikanaji wa mafuta na kuyasafirisha mpaka Mwanza, mtambo huo haukutumika kuzalisha umeme hata siku moja ndani ya miezi 12 ya mkataba, zaidi ya masaa ishirini tu kwa ajili ya majaribio kabla ya mtambo kukabidhiwa kwa Serikali. Kwa kifupi ni kwamba kampuni hiyo ililipwa kiasi dola za kimarekani milioni 1.7 (sawa na takriban kiasi cha shilingi bilioni mbili na nusu) kwa mwezi za bure, bila kuzalisha umeme wowote. Ili wananchi waone kwamba Serikali yao ina uchungu na rasilimali za umma, nashauri Taarifa ya Serikali lieleze hatua za uwajibikaji kwa hasara hii ya takriban dola la Kimarekani milioni 20. Lakini vilevile, ili kuondoa uwezekano wa kujengeka dhana kwamba Serikali yetu haiko makini, nashauri Taarifa ya Serikali ielezee ni kwa vipi tena Serikali imenunua na kupeleka mtambo wa kuzalisha umeme kwa kutumia mafuta mahali kulekule Mwanza. Kama hadi sasa ni shida na ni gharama kubwa kupata mafuta ya kuendesha mtambo wa IPTL hapa Dar es Salaam, kiasi kwamba mtambo huo unazalisha umeme chini ya nusu ya uwezo wake, inakuwaje sio shida wala gharama kubwa kupata mafuta hayo hayo mazito na kuyasafirisha Mwanza ili kuendesha mtambo wa kuzalisha megawati 60? Kuna jambo gani jipya limebadilika tangu mradi kama huu ushindikane kutekelezwa Mwanza kutokana na gharama kubwa za mafuta na hadi sasa tunaingia tena kwenye mradi kama ule wa kuzalisha umeme kwa mafuta?
4. Kama unavyofahamu, Mheshimiwa Waziri, zaidi ya asilimia 80 ya umeme wa Gridi unazalishwa kwenye upande wa Mashariki mwa nchi yetu (hasa katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam na Tanga) na katika Mkoa wa Iringa, lakini wateja wa umeme huo wametapakaa nchi nzima. Limekuwepo tatizo la muda mrefu la uchakavu na udogo wa njia kuu ya kusafirisha umeme kutoka Iringa hadi Shinyanga na kutoka Shinyanga hadi Geita. Njia iliyopo sasa haina uwezo wa kusafirisha umeme unaotoshelelesha mahitaji ya wateja na haijakarabatiwa wala kupanuliwa kwa muda mrefu. Iliahidiwa kwamba mradi mkubwa wa kukarabati njia hiyo utakuwa umekamilika itakapofika mwaka 2005, lakini hadi sasa mradi huo haujaanza. Ingependeza kama Taarifa ya Serikali ingeelezea hatua zinazochukuliwa ili miradi hiyo muhimu ianze mapema. Lakini pia, Mheshimiwa Waziri, nashauri kwamba Taarifa ya Serikali iwaelimishe Watanzania kuhusu hoja, busara au utaalamu wa kuendelea kununua na kukodisha mitambo ya kuzalisha umeme jijini Dar es Salaam wakati njia ya kuusafirisha umeme wenyewe, hasa kwenda kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, haijakarabatiwa na umeme haufiki kwa kiwango cha kuridhisha na takriban asilimia 20 ya umeme unaozalishwa unapotea njiani, na kusababisha hasara kubwa, kutokana na uchakavu wa njia za usafirishaji umeme.
5. Taarifa zilizopo ni kwamba mtambo wa kusafisha gesi kisimani Songosongo, uliojengwa mwaka 1996, umeanza kuelemewa na kama hatua za haraka hazijachukuliwa, miradi mipya ya kuzalisha umeme iliyotangazwa hivi karibuni – ya Megawati 100 Ubungo, Megawati 45 Tegeta na Megawati 240 Kinyerezi – inaweza isipate gesi ya kutosha, na kwa maana hiyo inaweza isitekelezwe kwa kiwango kinachotarajiwa. Nashauri pia Serikali ifafanue ni kwa vipi, licha ya kujulikana kwa tatizo hili Serikalini muda mrefu, bado mitambo mipya ya kuzalisha umeme ya karibu shilingi bilioni 400 (Ubungo, Kinyerezi, Tegeta) inapangwa kununuliwa na kukodishwa wakati kuna hatari kubwa ya kukosekana kwa gesi ya kuiendesha kwa ukamilifu.
6. Mheshimiwa Waziri, kama unavyojua, TANESCO, kwa miaka kadhaa sasa, imekuwa na kesi nyingi, aidha ikishtaki au ikishtakiwa. Ipo fursa kupitia Taarifa ya Serikali Bungeni kwa wananchi kujulishwa ni kiasi gani cha fedha kimetumika katika miaka mitano iliyopita kuwalipa wanasheria binafsi kuendesha kesi hizi na ni wanasheria gani waliotumiwa na TANESCO kuiwakilisha kwenye mashauri yaliyotokea katika miaka mitano iliyopita na yanayoendelea sasa. Kwa kuwa kuna maswali mengi kwenye jambo hili, nashauri wananchi pia wajulishwe kama zilitangazwa tenda ya kupata wanasheria binafsi wa kutoa huduma za kisheria kwa TANESCO kama Sheria ya Manunuzi ya Umma inavyotaka. Nashauri pia Taarifa ya Serikali Bungeni ionyeshe ni jitihada gani zimefanyika na ni kiasi gani cha fedha kimetumika kujenga uwezo wa wanasheria waajiriwa wa TANESCO na ni kwa kiasi wanashirikishwa katika maamuzi makubwa yanayohusu kesi kubwa za Shirika.
7. Kuhusu shauri la Dowans, Watanzania wameshuhudia kioja cha Mawaziri wa Serikali kujibizana na kupingana kwenye magazeti kuhusu malipo ya tuzo ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi (ICC) kwa Kampuni ya Dowans. Taarifa ya Serikali Bungeni kuhusu jambo hili ni muhimu ili kuweka bayana kwa Watanzania kwamba ni katika wakati gani, kwa njia gani na kwa jinsi gani Serikali inawasiliana na umma ili kuondoa mkanganyiko kwa wananchi na sisi Wabunge kuhusu msimamo wa Serikali kwenye masuala mbalimbali.
8. Mheshimiwa Waziri, mnamo tarehe 6 Januari 2011, ulizungumza na waandishi wa habari na kuelezea kwamba Serikali inajipanga kuilipa Dowans tuzo iliyoamuliwa na ICC. Lakini, kwa kuwa mzigo huu ni mzito kwa umma, kumekuwa na fikra, ikiwemo pendekezo la Kamati ya Wabunge Wote wa CCM, kwamba ni muhimu kutumia mianya ya kisheria iliyopo kupinga rasmi kutekelezwa kwa hukumu hiyo. Kwa kuwa hukumu hiyo imekwishasajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania kitambo sasa, na kwa kuwa kila siku inayopita, kwa mujibu wa hukumu ya ICC, faini kwa TANESCO inaongezeka kwa shilingi milioni 17. Nashauri Taarifa ya Serikali ibainishe ni lini hasa Serikali inatarajia kupeleka Mahakamani pingamizi la utekelezaji wa hukumu hii. Na hatua hii inamuweka wapi Mwanasheria Mkuu wa Serikali, pamoja na tamko lako la tarehe 6 Januari 2011, kwamba kupinga utekelezaji wa hukumu ya ICC ni kupoteza muda.
9. Kwenye viambatisho vya hukumu ya ICC, kama ilivyosajiliwa Mahakama Kuu ya Tanzania, zipo nyaraka zinazoonyesha kwamba mwanasheria aliyeishauri TANESCO kuvunja mkataba na Dowans – kwa kusema kwamba sio mkataba halali na kwamba hakuna madhara ya kisheria kuuvunja – ndiye huyo huyo pia aliyeishauri Benki ya STANBIC kutoa mkopo wa dola za Kimarekani milioni 20 kwa Dowans – kwa kusema kwamba ni kampuni halali, inakopesheka na ina mkataba halali na TANESCO. Na ndiye huyo huyo aliyeiwakilisha TANESCO kwenye kesi iliyofunguliwa na Dowans, kesi ambayo imetokana na ushauri wake, na, baada ya hukumu, ndiye huyo huyo, kwa mujibu wa maelezo yako Mheshimiwa Waziri ya terehe 6 Januari 2011, aliyetoa ushauri kwamba hakuna njia nyingine zaidi ya kuilipa Dowans. Mheshimiwa Waziri, jambo hili likibaki hivi hivi bila maelezo inaweza kujengeka sura kwamba Serikali ilikosa umakini kwenye jambo hili zima na maadili hayakuzingatiwa. Itakuwa vyema kama Taarifa ya Serikali ikaeleza ni wanasheria gani waliotumiwa na TANESCO kwenye kila hatua ya shauri la Dowans, kuanzia kwenye ushauri kabla ya kuvunjwa kwa mkataba hadi ushauri baada ya kesi kuamuliwa, na kiasi cha fedha walizolipwa kwa kila hatua, na utaratibu gani ulitumika kuwapata.
10. Vilevile, ili kuwaondoa wasiwasi Watanzania, ambao baadhi yao wanaamini kwamba TANESCO ilishindwa kwenye kesi ya Dowans kutokana na upungufu wa weledi kwa wanasheria walioiwakilisha kwenye kesi hiyo, nashauri Taarifa ya Serikali ielezee utaratibu uliotumika kuwapata wanasheria wanaoiwakilisha Serikali na TANESCO kwenye mashauri yaliyofunguliwa na Benki ya Standard Chartered kwenye Mahakama ya Kimataifa kama nilivyoyaelezea mwanzoni mwa barua yangu. Mheshimiwa Waziri, utaniwia radhi kama baadhi ya mambo niliyokuandikia tayari unayafahamu. Niwie radhi pia kwa kuandika maelezo marefu kwenye kila kipengele. Dhamira yangu ni kutaka kueleweka katika kile ninachokusudia katika kuandika barua hii, ambacho kwanza ni kutoa ushauri, kama wajibu wangu wa Ubunge unavyonitaka na pili ni kutoa ombi kwa Serikali kupitia kwako. Ninachoomba ni kwamba wananchi nao, kupitia Taarifa rasmi ya Serikali Bungeni, wapatiwe fursa ya kuzijua kwa kina changamoto hizi katika sekta ya nishati na jinsi Serikali inavyozishughulikia ili imani yao kuhusu uwezo wa Serikali yao kulishughulikia tatizo la umeme nchini isizidi kuporomoka. Naamini kwamba kwa taarifa hii, tutafungua ukurasa mpya kwa kuondoa siasa kwenye maamuzi na mijadala inayohusu sekta hii na kuweka uwazi kwenye mwenendo mzima wa uendeshaji wa sekta ya nishati, ikiwemo mikataba ya uzalishaji wa umeme. Nichukue fursa hii kukupongeza kwa kuteuliwa tena kushika wadhifa wa Waziri wa Nishati na Madini. Nakuahidi ushirikiano wangu wakati wote. Kwa heshima na taadhima, naomba kuwasilisha,
January Makamba (MB)
Nakala:
Mheshimiwa Mizengo Pinda (MB)
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dar es Salaam.
Mheshimiwa Anna Makinda (MB)
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dodoma.
Mheshimiwa William Lukuvi (MB)
Waziri wa Nchi – Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge)
Dar es Salaam.
Dk. Thomas Kashillila
Katibu wa Bunge
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dodoma.
No comments:
Post a Comment